NBC yachangia milioni 15 ujenzi wa Uwanja wa Golf Iringa, RC aipongeza

0
66

Benki ya Taifa ya Biashara NBC, Novemba 13, 2022 imeidhamini Club ya Golf ya Mkwawa University Golf Club Shilingi Milioni 15 , kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Golf ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali na Mkoa wa Iringa kwa Ujumla katika kutangaza utalii wa Kusini maarufu kama ” UTALII KARIBU KUSINI ” ambao maadhimisho yake yamefungwa leo hii katika viwanja vya Kihesa Kilolo mkoani humo.

Akizungumza baada ya kupokea mfano wa Hundi ya Milioni 15 kutoka kwa Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wateja Wadogo Benki ya NBC Bwn. Elibariki Masuke , Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendego ameipongeza Benki ya NBC kwa jinsi inavyojitoa katika kuunga mkono masuala mbalimbali ya kijamii pamoja na michezo

” Hakika Benki ya NBC tunajivunia sana uwepo wenu , asante sana kwa jitihada zenu katika kukuza sekta ya michezo nchini lakini pia kwa umuhimu mkubwa niwashukuru sana kwa kuiunga mkono klabu yetu ya Golf ya ” Mkwawa University Golf Club ” asanteni sana kianzio icho kitasaidia sana katika kuendeleza mchezo wa Golf hapa Iringa na moja kwa moja kutengeneza fursa zaidi za utalii asanteni sana ” alimalizia.

Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wateja wadogo wa Benki ya NBC Bwn. Elibariki Masuke amesema kuwa “Kama kawaida yetu Benki ya NBC tunapenda sana kuunga mkono sekta ya michezo hapa nchini , kama mnavyojua sisi ni wadhamini wakuu wa Ligi ya mpira wa miguu maarufu kama NBC PREMIER LEAGUE lakini tumekua tukiendesha mashindano ya Marathon Maarufu kama NBC DODOMA MARATHON ambapo fedha zinazopatikana katika mashindano hayo ya mbio huenda moja kwa moja kuwasaidia akina mama wenye matatizo ya kansa ya Kizazi.”

“Kwahiyo tupo hapa kujumuika na wana Iringa hasa katika tamasha hili kubwa lililofungwa leo Tamasha la ” Karibu Utalii Kusini ” ambalo limehusisha watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na sisi tumekuja kama wadhamini wa uwanja wa Golf ambapo tunaamini ukiwepo uwanja wa Golf hapa basi utavutia watalii zaidi na zaidi kwa maana Watalii watapata sehemu nzuri ya kujiburudisha baada ya kumaliza shughuli zao mbalimbali huko hifadhini ” Alimalizia .

 

Kwa upande Mwingine , akizungumza kwa Niaba ya Bwn. Edmund Mkwawa Mwenyekiti wa Mkwawa University Golf Club , Yohannes Chavala ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Klabu hiyo ameipongeza Benki ya NBC kwa mchango wao uliotukuka wa milioni 15 , na kuongezea kuwa ujenzi wa uwanja huo wa Golf utavutia watalii wengi na kukuza Utalii wa Kusini na Tanzania nzima kwa Ujumla.

 

 

 

Send this to a friend