Chama cha NCCR Mageuzi kimemtuhumu aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia kuuza mali za chama kiholela ikiwemo nyumba, kwa maslahi binafsi.
Akizungumza na Swahili Times Faustine Sungura ambaye ametoa taarifa hiyo kwa niaba ya katibu mkuu wa chama, amesema Mbatia aliuza nyumba mbili mwaka 2016 kwa gharama ya TZS milioni 67 na TZS milioni 68 pamoja na kupora shamba la chama lenye ukubwa wa ekari 56 wakati akihudumu kama mwenyekiti wa chama hicho kwa kushirikiana na rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Msabaha.
“Mbatia ni mwizi amepora myumba za chama na ndiyo maana tulimfukuza kwenye chama chetu tukamfungulia jalada kule Mbweni,” ameeleza huku akidai wakati wa kufungua jalada hilo, Ofisi ya RCO wa Kinondonu ilijaribu kumlinda Mbatia lakini IGP aliamuru jalada hilo lifunguliwe.
“Ushahidi upo, taarifa ya CAG imemtaja amepora nyumba za chama ni kweli, mezani wanapeleka nyaraka kama hizo polisi, Mbatia anaenda anawapa hela wananyofoa wanapeleka vitu ambavyo havijakamilika kwa DPP na DPP akiona haoni ushahidi anasema hamna kesi,” ameeleza Sungura.
Aidha, amesema hatua walizochukua kwa sasa ni kuweka wazi tuhuma hizo pamoja na kuwapa barua ya kuondoka kwenye nyumba wale wote waliouziwa nyumba hizo kinyemela.