
Chama cha NCCR- Mageuzi kimetangaza kwamba hakina mpango wa kushirikiana na chama chochote katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kimethibitisha kushiriki kikamilifu katika kinyang’anyiro hicho kikiwa peke yake.
Msimamo huo umetolewa na Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Ambar Haji Khamis Jumanne, Februari 18, 2025, mbele ya waandishi wa Habari akisisitiza kuwa chama hicho kitaingia kwenye uchaguzi huo bila kushirikiana na chama kingine chochote, tofauti na ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2015.
“Sisi NCCR- Mageuzi tuko peke yetu na tutaendelea kuwa peke yetu mpaka hapo vikao halali vya chama vitakavyoona vinginevyo. [..] Lakini kwa sasa sisi umoja tulishauvunja, na tuliuvunja Dodoma kwenye mkutano mkuu, hatutaki umoja,” amesema.
Ameongeza, “Madhara yaliyotukuta 2015 ni makubwa mpaka leo hatujapona. Tuliingia kwenye UKAWA tukiwa na wabunge wanne tukatoka na mbunge mmoja, sisi hatukufaidika chochote na umoja ule.”
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, NCCR Mageuzi kilikuwa miongoni mwa vyama vya upinzani vilivyoshirikiana kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), pamoja na CHADEMA, CUF, na NLD