Nchi za Afrika zinazoongoza kwa raia kumiliki bunduki

0
33

Kuenea kwa silaha barani Afrika kunazidi kuwa tishio kubwa kwa usalama, uthabiti, na maendeleo ya bara hilo, licha ya uwepo wa sheria kali zinazolenga kudhibiti umiliki wa bunduki miongoni mwa raia.

Ripoti ya Small Arms Survey inaonyesha kuwa Afrika inaongoza kwa soko kubwa zaidi la silaha haramu duniani, hali inayochangiwa na upatikanaji rahisi wa silaha, haswa zile zilizoachwa baada ya vita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwa na ongezeko kubwa la silaha zinazoingia mikononi mwa raia, kutoka silaha milioni 650 mwaka 2006 hadi silaha milioni 857 mwaka 2017.

Miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya umiliki wa silaha kwa raia ni Afrika Kusini, Nigeria, Ethiopia, Libya, na Sudan. Sababu kuu zinazoelezwa ni pamoja na changamoto za kiusalama, kushindwa kwa vyombo vya sheria kutekeleza wajibu wao, na urahisi wa kupata silaha kama bunduki aina ya AK-47, ambazo huuzwa kwa gharama ya chini sana katika baadhi ya mataifa.

Changamoto hii imeongeza muda na migogoro katika maeneo kama Sahel, Afrika ya Kati, na Pembe ya Afrika, hali ambayo husababisha mamilioni ya watu kupoteza makazi yao na kuunda janga la kibinadamu linalojumuisha njaa, umasikini, na ukosefu wa huduma za msingi.

Licha ya juhudi za nchi nyingi za Afrika kutunga sheria kali, ukosefu wa rasilimali za kutosha na udhaifu wa taasisi husika vimekuwa vikwazo vikubwa katika kudhibiti ueneaji wa silaha haramu.

Hali hii inatoa wito kwa jumuiya za kimataifa, serikali za Afrika, na wadau wengine kushirikiana katika kushughulikia changamoto ya silaha haramu kwa njia ya sera madhubuti, juhudi za kuimarisha mifumo ya usalama, na kuondoa mizizi ya migogoro inayoendelea barani.

Zifuatazo ni nchi za Kiafrika zenye viwango vya juu zaidi vya umiliki wa bunduki miongoni mwa raia;

 

  1. Nigeria: 6,200,000
  2. Afrika Kusini: 5,350,000
  3. Misri: 3,930,000
  4. Angola: 2,980,000
  5. Sudan: 2,770,000

Chanzo: Business Insider

Send this to a friend