Ndege ya mizigo ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imesafirisha jumla ya tani 2,084.7 za mizigo kuanzia Julai, 2023 hadi Machi mwaka huu ikichangia asilimia 41 ya tani 5,034.2 za mizigo zilizosafirishwa ndani na nje ya nchi katika kipindi hicho.
Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba tani 54 iliwasili nchini Juni, 2023, ambapo husafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na vituo vya Nairobi na Dubai mara moja kwa wiki, pamoja na vituo vingine ambavyo wateja wenye mizigo hukodi vikiwemo vya Mumbai (India), Eldoret (Kenya), Mombasa (Kenya), Bujumbura (Burundi), Kinshasa (Kongo DRC), Bangui (Cetral Afrika), N’Djamena (Chad), Entebbe (Uganda), na Lusaka (Zambia).
Katika hotuba ya Wizara ya Uchukuzi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni imebainisha ongezeko la usafirishaji mizigo kuwa ni sawa na asilimia 87.78 ikilinganishwa na tani 2,680.9 zilizosafirishwa katika kipindi kama hicho katika mwaka wa Fedha 2022/23.
Hotuba hiyo imeeleza kuwa Serikali imeiwezesha ATCL kuanza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mizigo katika viwanja vya Ndege vya JNIA, KIA na Songwe ili kukuza biashara ya usafirishaji wa mizigo pamoja na ubora wa bidhaa zinazosafirishwa, na kwamba mchakato wa kumpata mkandarasi upo katika hatua za mwisho.