Ndugu wajiua baada ya baba yao kumpa shamba mke wake wa zamani

0
40

Kisa cha kustaajabisha kimeripotiwa katika kijiji cha Kapsilibwa huko Sagamian, Kaunti ya Narok nchini Kenya baada ya ndugu wawili kukatisha maisha yao kwa kujinyonga kutokana na mzozo wa ardhi katika familia yao.

Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa Vincent Kipkorir Koech (19) na Gilbert Kibet Koech (17), waliamua kufanya kitendo hicho baada ya baba yao, David Towett kumgawia mke wake wa kwanza shamba, mke ambaye hivi karibuni alikuwa amerejea nyumbani baada ya kuachana na Towett miaka kadhaa iliyopita.

“Sababu ya kukubali kujiua ni kwamba baba yao alikuwa na wake wawili na kwamba yule mkubwa ambaye alikuwa ametalikiwa miaka mingi iliyopita alirudi nyumbani na baba huyo aliamua kumpa kipande cha ardhi,” imesema ripoti ya polisi.

Imeongeza kuwa “hatua hiyo haikuungwa mkono na ndugu hao wawili walioaga dunia ambao hata walitishia kuua familia nzima ya kambo na baba yao.”

Aidha, taarifa hiyo ya polisi imeeleza kwamba wawili hao walikuwa na rekodi za uhalifu hapo awali ikiwa ni pamoja na wizi katika makanisa mawili katika eneo hilo.

Polisi wamefanya uchunguzi katika eneo la tukio huku miili ya ndugu hao ikihifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Longisa kwa ajili ya uchunguzi.

Send this to a friend