NEC: Spika Ndugai hakututaarifu kuhusu Jimbo la Ndanda kuwa wazi

0
20

Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mvutano kuhusu uhalali wa ubunge wa Cecile Mwamba katika Jimbo la Ndanda, Mtwara, baada ya kujivua uanachama wa chama kilichomdhamini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kujiunga Chama cha Mapinduzi (CCM).

Sintofahamu hiyo iliibuka baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kumrejesha bungeni na kumtambua Mwambe kama mbunge halali licha ya kuwa alihama chama na kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mbunge kwa mujibu wa sheria.

Akieleza sababu za kuendelea kumtambua Mwambe kama mbunge halali, Spika Ndugai alisema mapema Mei mwaka huu kuwa, hakuwahi kuandikiwa barua na mbunge huyo kuwa mejiuzulu, na barua ya CHADEMA iliyowasilishwa bungeni kueleza Mwambe asitambuliwe kama mbunge haikuambatanishwa na nyaraka za msingi hivyo alisema haina mantiki.

Aidha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa haijapokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuwaeleza kwa maandishi kuhusu Jimbo la Ndanda kuwa wazi kama ambavyo sheria inataka.

Emanuel Kawishe, Mkurugenzi wa Huduma za Sherua wa NEC ameongeza kuwa, hata kama spika angewaandika barua hiyo, uchaguzi mdogo kwenye jimbo hilo usingefanyika kwani sheria inaeleza kuwa, miezi 12 kuelekea bunge kuvunjwa, hakutakuwa na uchaguzi mdogo wa wabunge na/au madiwani.

Ameongeza kuwa mbunge anapoondoka kwenye chama kimoja kuna taratibu za kufuatwa ikiwemo chama kutoa taarifa bungeni kuhusu kuondoka kwa mbunge, na endapo taratibu hizo zisipofuatwa, mbunge aliyefukuzwa au kujiondoa inawezekana akaendelea kuwepo.