NEC yaitangaza kampuni inayochapisha karatasi za kupigia kura za Uchaguzi Mkuu 2020
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo si za kweli kuhusu mchakato wa kumpata mzabuni wa uchapishaji wa karatasi za kupigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
NEC imekanusha taarifa hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika na kueleza kuwa mchakato wa kumpata mzabuni ulifuata kanuni, taratibu na sheria za nchi.
Mamlaka hiyo imesema kuwa ufunguzi wa zabuni ulifanyika Aprili 8, 2020 na jumla ya makampuni matatu yalishiriki ambapo yote yalikuwa ya nje ya nchi. Kampuni hizo ni M/s Ren-Form CC ya Afrika Kusini, M/s Elliams Product Limited ya Kenya na M/s Al Ghurair Printing and Publishing LCC ya Dubai.
Baada ya zabuni kufunguliwa na kufanyiwa uchambuzi, Mzabuni M/s Ren-Form CC wa Afrika Kusini alitangazwa kuwa mshindi, na hivyo mzabuni aliyetajwa na Mnyika kwa jina la Jamana Printers hakuhusika popote kwenye mchakato huo.
NEC imeutaka umma wa Watanzania kupuuza taatifa hiyo potofu kwanj inalenga kuleta taharuki katika jamii. Mamlaka hiyo imeongeza kuwa maandalizi ya vifaa vya uchaguzi yamekamilika, na sasa vinasambazwa katika maeneo husika.