
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imewatangazia wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa imeongeza siku mbili za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambazo ni tarehe 24 na 25 Machi, 2025 ili kuwezesha wananchi wote kujiandikisha.
NEC imesema inawapongeza wananchi wa Mkoa huo kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mara ya kwanza, kuboresha au kuhaisha taarifa zao na kupata kadi mpya kwa wale ambao kadi zao zimepotea au zimeharibika.
Aidha, NEC imesema kutokana na mwitikio mkubwa imechukua hatua za kuongeza mashine za bvr kits pamoja na watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi, na kwamba hatua hiyo imewezesha zoezi hilo kuongeza kasi na kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote.
Imeongeza kuwa zoezi hilo halihusishi ubadilishaji wa kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 kwa kuwa kadi hizo ni halali na zitaendelea kutumika kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
NEC imeongeza kuwa ni kosa kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kujiandikisha zaidi ya mara moja, na kwamba atakayethibitika atakabiliwa na faini isiyopungua shilingi laki tatu au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja