NEC yataka wanaopita bila kupingwa wapigiwe kura

0
43


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imependekeza wagombea ubunge na udiwani wanaopita bila kupingwa katika chaguzi wapigiwe kura.

Pendekezo hilo limetolewa na Jaji Rufaa (Mst), Semistocles Kaijage wakati akiwasilisha ripoti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassa.

Jaji Kaijage ametoa pendekezo hilo ambalo huenda likaondoa utaratibu wa sasa ambao mgombea ubunge au udiwani anapopita bila kupigwa (bila kuwepo mshindani kutoka chama kingine), basi inahesabika ameshinda, na anakuwa mbunge au diwani mteule.

Mapendekezo mengine aliyowasilisha ni pamoja na sheria za uchaguzi zitafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili ili Watanzania wengi waweze kuzielewa, na serikali kuziwezesha kifedha asasi zinazotoa elimu ya mpigakura kwa wananchi.

Aidha, NEC imependekeza uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa usimamiwe na mamlaka moja na sheria ya taifa ya uchaguzi na sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa ziunganishwe ili kurahisisha utekelezaji wa sheria hizo.

Kwa upande wake Rais Samia ameipongeza NEC kwa namna ilivyofanikisha uchaguzi huo na kusema ulifanyika vizuri kwa kuhakikisha uwepo wa vituo vingi vya kupigia kura na kuepusha misongamano, uwepo wa vifaa vya kutosha na kwa mara ya kwanza kuhakikisha uwepo wa karatasi nundu kwa ajili ya wapigakura wenye ulemavu wa kuona.

Pia amesisitiza wanawake kujitokeza zaidi kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa kwani katika uchaguzi uliopita kati ya wagombea na wagombea wenza 30, wanawake walikuwa ni saba tu.

Aidha, amesema kuwa mapendekeo yote yaliyowasilishwa ni ya msingi hivyo serikali itayapitia kuona namna ya kuyafanyia kazi.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 28, 2020, wapigakura zaidi ya milioni 29.7 walindikishwa lakini waliojitokeza kupiga kura ni zaidi ya milioni 15.9 sawa na asilimia 50.72.

Send this to a friend