NEC yateua wagombea 58 kwenye uchaguzi wa Ubunge na Udiwani mwezi ujao

0
52

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeteua wagombea 58 kutoka vyama 17 vya siasa kuwania nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Mbarali wilayani Mbarali pamoja na nafasi za Udiwani katika Kata sita za Tanzania Bara, uchaguzi utakaofanyika Septemba 19 mwaka huu.

Katika taarifa iliyotolewa leo na NEC wagombea 70 walichukua fomu za uteuzi ambapo kati yao, wagombea 58 waliteuliwa na wagombea 12 hawakurejesha fomu za uteuzi. Kati ya wagombea 58 walioteuliwa, wagombea 44 sawa na asilimia 75.8 ni wanaume na wagombea 14 sawa na asilimia 24.2 ni wanawake.

Aidha, vyama vilivyotoa wagombea hao ni; ACT- Wazalendo, AAFP, ADA- TADEA, ADC, CCK, CCM, CUF, Demokrasia- Makini, DP, TLP, NCCR- Mageuzi, NLD, NRA, SAU, UDP, UMD na UPDP.

“Pamoja na Jimbo la Mbarali, Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo ni; Nala iliyopo halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo,” imesema taarifa.

Send this to a friend