
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limezitaka shule na wanafunzi wote wanaotarajia kufanya mtihani wa Darasa la Saba kuepuka vitendo vya udanganyifu, likisisitiza kuwa halitasita kufuta matokeo ya yeyote atakayebainika kushiriki katika vitendo hivyo.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Mohammed amesema jumla ya wanafunzi milioni 1.17 wanatarajiwa kufanya mtihani huo utakaofanyika Septemba 10 na 11, 2025.
“Ni matarajio yetu kwamba wanafunzi watajiepusha na vitendo vya udanganyifu, na watazingatia miongozo na kanuni za mitihani. Baraza halitarajii kuona mwanafunzi yeyote anajihusisha na vitendo vya udanganyifu kwani, mwanafunzi atakayebainika kufanya hivyo, matokeo yao yatafutwa kwa mujibu wa kanuni,” amesema.
Aidha, Baraza limewataka wananchi kutoa taarifa haraka pindi watakabaini vishiria vya hujuma au udanganyifu dhidi ya mitihani hiyo.








