NECTA yawafutia matokeo wanafunzi 31

0
47

Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza kufuta matokeo ya watahiniwa 31, waliofanya mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2023 baada ya kubainika kufanya udanganyifu.

Ameyasema hayo Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Mohammed wakati akitangaza matokeo hayo ya mitihani iliyofanyika Septemba 13 hadi 14, mwaka huu ambapo pia ameeleza kuwa watahiniwa walioshindwa kufanya mitihani hiyo watapewa nafasi ya kurudia mitihani yao mwakani 2024.

“Baraza la mitihani limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 360 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo. Hivyo watahiniwa hawa wamepewa fursa ya kurudia kufanya mtihani huu mwaka 2024 kwa mujibu wa kifungu cha 32 (1) cha kanuni za mitihani,” amesema.

NECTA imebainisha kuwa ufaulu wa jumla umepanda kwa asilimia 0.96 na kufikia asilimia 80.6, ambapo watahiniwa milioni 1,092,960 ya watahiniwa wote wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C.

Tazama hapa matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba mwaka 2023

Aidha, limesema ufaulu wa somo la Kiswahili ni asilimia 88 ambapo zaidi ya theluthi mbili wamepata gredi A na B, huku ufaulu wa somo la Kiingereza ni asilimia 34.35, na upande wa somo la hisabati ufaulu umeshuka kwa asilimia 4.46 na kufikia asilimia 48.83 ikilinganishwa na mwaka jana.

Vilevile, amesema takwimu zinaonesha ufaulu wa somo la Sayansi umepanda kwa asilimia 2.5 na kufikia asilimia 74 akibainisha kuwa ubora wa ufaulu katika somo la Sayansi na Teknolojia umeongezeka kwa watahiniwa waliopata daraja la A na B hadi asilimia 28.11 ikilinganishwa na asilimia 26.32 ya mwaka jana.