New Zealand yatangaza kudhibiti corona, wananchi watakiwa kuishi kama kawaida

0
41

Serikali ya New Zealand imetangaza kuwa imedhibiti maambukizi ya virusi vya corona nchini humo, na itaondoa vizuizi vyote vilivyokuwa vimeweka kukabiliana na maambukizi ya Covid-19.

Waziri Mkuu, Jacinda Ardern amesema kuwa vizuizi katika maeneo ya mipakani vitaendelea kuwepo, lakini shughuli nyingine za kiuchumi, kijamii, usafiri wa umma zitaruhusiwa kurejea kama kawaida bila watu kutakiwa kukaa mbalimbali.

“Licha ya kuwa kazi haijaisha, hakuna wa kukataa kwamba hii ni hatua kubwa, asanteni sana New Zealand,” amesema Ardern akizungumza na waandishi wa habari.

Hatua hiyo imeifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi za awali kuthbitisha kuwa zimedhibiti maambukizi ya virusi hivyo vinavyoendelea kuisumbua dunia.

Kwa siku 75 nchi hiyo ilikuwa imeweka vizuizi mbalimbali kukabiliana na corona ikiwa ni pamoja na ‘lockdown’ ambapo biashara nyingi zilifungwa na watu wote isipokuwa watu wachache waofanya kazi muhimu sana walitakiwa kusalia majumbani.

“Baada ya siku 75 sasa tupo tayari,” amesema kiungozi huyo wakati akieleza kuwa amri ya watu kukaa mbalimbali itaondolewa leo usiku, na nchi itaondoka katika ngazi namba moja (level 1) ya tahadhari kwenda namba 2.

Kwa sasa hakuna mgonjwa yeyote wa corona nchi humo, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu ugonjwa huo ulipoingia Februari 2020 ambapo wizara ya afya iliripoti jumla ya visa 1,154 na vifo 22.

Kiongozi huyo amepongezwa kwa uongozi wake makini kwa namana alivyokabiliana na janga hilo, hivyo kufanya umaarufu wake kukua.

Send this to a friend