Ng’ombe alizotoa Rais Samia mradi wa BBT zaibwa

0
50

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza, Paulo Chacha ametoa agizo la kufanyika uchunguzi kwa wanafunzi 60 wanaopata mafunzo ya ufugaji katika shamba la mifugo la Mabuki wilayani humo kutokana na tuhuma za upotevu wa ng’ombe sita kati ya 600 waliotolewa kwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya programu ya Jenga Kesho Bora (BBT).

Wanafunzi hao ni wahitimu wa vyuo wanaopatiwa mafunzo ya ujuzi katika ufugaji na unenepeshaji wa mifugo kupitia programu hiyo. Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, kila mmoja anatarajiwa kupewa ng’ombe 10 kwa ajili ya kuwanenepesha na baadaye kuuza, na kisha kubaki na faida itakayopatikana.

Aidha, Mkuu wa Wilaya, Paulo Chacha, amebainisha kwamba Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika katika wizi wa ng’ombe hao. Kupitia jitihada za ufuatiliaji, ng’ombe wanne wamerejeshwa, huku wawili wakiwa bado hawajapatikana.

Chacha amesisitiza kuwa uchunguzi utaendelea ili kubaini mtandao uliohusika katika wizi wa ng’ombe hao na kuwafikisha mbele ya sheria, lengo likuwa ni kumaliza vitendo vya wizi katika shamba hilo la mifugo na kuhakikisha kuwa programu ya ‘Jenga Kesho Bora’ inatekelezwa kwa ufanisi.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend