Nigeria: Gharama za maisha zapelekea wananchi kutumia magari yao kufanyia biashara

0
12

Kutokana na kuendelea kudorora kwa uchumi wa Nigeria, wananchi nchini humo wameendelea kubuni njia zitakazorahisisha upatikanaji wa pesa kwa kugeuza magari yao kufanyia biashara.

Magari hayo yametumika kufanya biashara mbalimbali kama vile kuuza nguo, viatu, vyombo vya jikoni, huku wakifungulia milango ya gari katika pembezoni mwa barabara kama njia ya kuwakaribisha wateja.

Vivyo hivyo, wengine wengi wamevutiwa na biashara ya usafirishaji wa watu wakitumia magari yao binafsi kutoa huduma za usafirishaji.

Kulingana na utafiti wa hivi karibuni, umebaini kuwa watu waliopoteza ajira zao wamekuwa wakijaribu njia mbadala za kujipatia kipato kwa kubadilisha magari yao kufanya biashara, ili kusaidia kugharamia gharama za mafuta na kuzuia magari yao kuoza kwa kukaa bila kutumika.

Aidha, gharama kubwa sana za kodi za maduka zimefanya iwe ngumu zaidi kwa wajasiriamali wanaotarajia kuanzisha biashara kukabiliana na hali hiyo ya kiuchumi, hivyo wanasema kwa kufanya hivyo kunaokoa gharama.

Hata hivyo, hali hiyo haiwalengi walioathiriwa na kupoteza kazi zao, kwani wale ambao hapo awali walikuwa na maduka ya kawaida sasa wanabadilisha biashara zao na kutumia magari yao kutokana na ongezeko kubwa la gharama za upangaji.

Send this to a friend