Nigeria kutoa mikopo kwa wanafunzi isiyo na riba
Bunge la Nigeria limepitisha muswada wa sheria unaotaka kuanzisha benki ambayo inaweza kutoa mikopo kwa wanafunzi katika taasisi za juu za masomo ambazo ni pamoja na vyuo vikuu na vyuo vya kati.
Muswada huo ni wa kwanza na wa aina yake nchini humo ambao ulipitishwa na mabaraza mawili ya Bunge siku ya Jumanne na inatarajiwa kutumwa kwa Rais Muhammadu Buhari kwa ajili ya kupata idhini ya mwisho.
Mfadhili wa muswada huo na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Femi Gbajabiamila, amesema kuwa Benki ya Elimu ya Nigeria itatoa mikopo isiyo na riba kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini humo.
Amesema iwapo muswada huo utatiwa saini kuwa sheria, inatarajiwa kuwawezesha wanafunzi kupata msaada zaidi wa kifedha kutoka serikalini.
Muswada huo unasema benki “itakuwa na mamlaka ya kuidhinisha na kutoa mkopo kwa waombaji waliohitimu. Pia itafuatilia akaunti/mfuko wa mkopo wa wanafunzi na kuhakikisha uzingatiaji kuhusiana na ulipaji.”
Benki za Nigeria zimekuwa zikitoa mikopo ya wanafunzi kwa wazazi wa wanafunzi pekee na yenye masharti magumu. Wanafunzi wenye uhitaji wamelazimika kuacha shule au kujishughulisha na kazi zisizo za kawaida ili kujilipia ada.