Nigeria kuzifunga akaunti za benki zilizotumika wakati wa maandamano

0
40

Benki Kuu ya Nigeria imepewa kibali na mahakama kuzifunga (freeze) akaunti 20 za benki zinazohusishwa kutumika wakati wa maandamano ya kupinga ukatili dhidi ya Polisi (END SARS) nchini humo.

Kibali hicho kilichotolewa Novemba 4 mwaka huu kinairuhusu benki hiyo kuziamuru benki sita za kibiashara kuziwekea zuio akaunti hizo kwa siku 90 zikisubiri kukamilika kwa upelelezi wa benki kuu. Hata hivyo baadhi ya akaunti hizo zinadaiwa kuwa zilizuiwa tangu Oktoba 20, 2020 kabla benki haijapata kibali cha mahakama.

Akaunti hizo zinamilikiwa na washiriki wa maandamano hayo yaliyoanza mwezi uliopita. Uamuzi huo umeiathiri pia Gatefield Nigeria Ltd., kampuni ya masuala ya umma ambayo ilichangisha fedha kuwawezesha waandishi wa habari wa kujitegemea kufuatilia maandamano hayo.

Wahusika wa akaunti hizo wametishia kufungua kesi mahakamani dhidi ya benki zao kwa madai kuwa akaunti zao zilifungwa pasi na kupewa taarifa jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Katika maandamano hayo yaliyoanza kwa amani na baadaye kugubikwa na vurugu na kuchukua sura ya kisiasa yalipelekea vifo vya raia 51 na polisi 22, serikali imesema.

Send this to a friend