Nigeria: Serikali yashikilia ndege binafsi ya Waziri kwa kujipatia mabilioni katika dili ya mafuta

0
67

Serikali ya Nigeria inaishikilia ndege ya kifahari ya aliyekuwa waziri wa mafuta wa nchi hiyo, Dan Etete kufuatia kuhusishwa kwake katika tuhuma za rushwa za dili la mafuta (OPL245) lenye thamani ya $1.3 bilioni (TZS 3.01 trilioni).

Ndege hiyo aina ya Bombardier 6000 jet (M-MYNA) alikamatwa Mei 29 mwaka huu mara tu ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Montréal-Trudeau nchini Canada ikitokea Dubai.

Kukamatwa kwa ndege hiyo kunatokana na kibali kilichotolewa na mahakama katika Jimbo la Quebec. Hata hivyo, kampuni ya Tabit Ltd ambayo inamiliki wa ndege hiyo alipewa hadi Juni 9 mwaka huu kukata rufaa kupinga kushikiliwa kwa mali yake.

Etete anadaiwa kuwa alinunua ndege hiyo kwa $57 milioni (TZS 132.5 bilioni) mwaka 2011.

Katika dili la mafuta, Etete anadaiwa kuwa alipewa $336 milioni (TZS 778.5 bilioni), na pia aliipa kampuni aliyokuwa akiimiliki kwa siri, Malabu Oil and Gas, sehemu ya haki katika kitalu kikubwa cha OPL 245.

Baada ya kifo cha Rais Sani Abacha, Etete alibaki na haki hizo kama raia wa kawaida hadi mwaka 2011 alipoziuza kwa kampuni ya mafuta ya Shell and Eni ambapo waliilipa serikali $1.3 bilioni.

Uchunguzi unaonesha kuwa $336 milioni ziliingia kwake kupia akaunti mbalimbali za benki na kwamba malipo ya kwanza aliyofanya ya $54 milioni yalikuwa kwa ajili ya ndege hiyo.

Mamlaka chini Nigeria zimemshtaki Etete kwa makosa mengine kama vile utakatishaji fedha kupitia dili la mafuta. Kiongozi huyo hayumo nchini Nigeria na mamlaka zimeanza mchakato wa kumrejesha ili afikishwe kizimbani.

Hata hivyo mtuhumiwa amekana mashtaka yote na kusema kuwa tuhuma hizo ni propaganda za kisiasa.

Send this to a friend