Njia 6 za kumsaidia mtoto kupenda hesabu

0
56

Somo la hisabati limejengeka miongoni mwa watu wengi kuwa ni somo gumu zaidi ambalo wanafunzi wengi hulichukia na hata kuongoza kufanya vibaya kwenye mitihani.

Kama mzazi, unaweza kuchangia kwa sehemu kubwa kuondoa dhana hii kwa kumfanya mtoto wako aelewe na kupenda somo hili tangu akiwa mdogo na mara baada ya vipindi vya shule.

Hizi ni njia 6 zitakazomsaidia mtoto kupenda hesabu;

1.        Unganisha michezo na Hesabu

Unaweza kutumia michezo kufanya hesabu ionekane rahisi. Tumia michezo ambayo inahitaji kuhesabu kama vile michezo ya kompyuta au programu za simu zenye michezo ya kufurahisha ikiwemo kufanya maswali na kujibu hisabati kwa haraka, michezo ya kuhesabu vitu au idadi ya hatua n.k.

2.        Kuwa Mfano Mzuri

Mtoto anaweza kujifunza kutoka kwako. Unaweza kumwonyesha jinsi unavyotumia hesabu katika maisha ya kila siku, kama vile kuhesabu pesa au kupika kwa kutumia vipimo sahihi.

3.        Kuwapa Changamoto za Kufurahisha

Badilisha mbinu za kufundisha ili kuwahimiza kutafakari na kujaribu kutatua maswali. Wape maswali madogo madogo ya kufanya ili wajisikie vizuri wanapofanikiwa. Lengo ni kuwasaidia kuendeleza ujuzi wao wa hisabati kwa kuwafanya wajisikie vizuri wanapotatua changamoto ngumu.

4.        Tumia vitu halisi

Tumia mifano halisi inayowahusu na ueleze jinsi hesabu inavyohusiana na maisha yao. Kwa mfano, unaweza kutumia vitu wanavyovipenda, mazingira ya nyumbani au kuhesabu pesa wanazopata kama njia ya kuwafundisha.

5.        Mhamasishe na umtie moyo

Kumsifia mtoto wako wakati anapofanya vizuri ni njia nzuri ya kumtia moyo kuendelea kujifunza. Usimfanye ajione aliyeshindwa au asiyeweza, kwani hali hiyo inaweza kujengeka akilini mwa mtoto na kushindwa kufanya vizuri.

6.        Weka Mazingira ya Kujifunza

Weka vitu vya kujifunzia hesabu katika mazingira yao ya kuchezea ili waweze kujifunza huku wakicheza.

Send this to a friend