Njia 8 za kufanikiwa na kuwashinda wengine kwenye usaili wa kazi

0
50

Ni ndoto ya kila kijana kuona anaitwa kazini mara baada ya kupeleka maombi ya kazi au usaili kwenye kampuni, shirika au serikalini.

Mara nyingi nafasi zinazohitajika huwa chache ukilinganisha na idadi ya watu wanaoomba, hivyo inakubidi kuwa tofauti au kufanya vitu vya ziada ili kupata nafasi hizo.

Ili kujitofautisha na waombaji wengine, ni muhimu kufanya baadhi ya mambo haya;

Jifunze vitu vingi kuhusu kampuni unayoomba kazi

Hii itakusaidia kwani utakuwa unajua kwa undani inashughulika na nini na unaweza kujitathimini uwezo wako na namna gani unaweza kutumia uzoefu wako kuifaidisha kampuni.

Ondoa woga
Kuwa mtulivu na ujibu maswali unayoulizwa kwa ufasaha huku ukijitahidi sana kutoa mifano ya mambo ambayo umepitia au umefanya katika kazi zako.

Toa mifano
Tumia mifano halisi ya jinsi ulivyotatua matatizo au jinsi ujuzi wako ulivyosaidia katika kazi ulizofanya awali. Hii inaweza kuonyesha uwezo wako wa kutumia maarifa yako katika mazingira ya kazi.

Mawasiliano Mazuri
Kuwa na mawasiliano mazuri ya moja kwa moja kwa kujibu maswali kwa uwazi na kujiamini. Unapozungumza, tumia lugha nzuri na uonyeshe tabia ya heshima.

Onyesha uwezo wa kujifunza
Onyesha uwezo wako wa kujifunza na kubadilika kwa kutumia mifano ya jinsi ulivyoshughulikia changamoto na kujifunza kutokana na makosa au uzoefu uliopita.

Kuwa Mwaminifu
Kuwa mwaminifu kuhusu uwezo wako na uzoefu wako wa kazi na uonyeshe mtazamo wako wa kweli.

Kuwa nadhifu
Unapokwenda kwenye usaili hakikisha unakuwa msafi kuanzia nywele hadi viatu. Nguo ulizovaa zinaweza kuwa si za bei ghali lakini zinapaswa kuwa safi, zenye rangi iliyotulia na yenye heshima.

Uliza maswali mazuri
Unaweza kuulizwa iwapo una swali la kuuliza. Hakikisha unauliza maswali mazuri ambayo yatafanya uache kumbukumbu nzuri kwa wanaokufanyia usaili. Usiulize maswali kama vile; mtanilipa shilingi ngapi, uliza kuhusu kampuni na shughuli wanazofanya.

Send this to a friend