Njia sita za kutambua na kuepuka matapeli mitandaoni

0
52

Watu mbalimbali wamekuwa wakilalamika juu ya kutapeliwa fedha zao mitandaoni na watu wanaodai kwamba wanafanya biashara.

Ili kukuwezesha wewe usitapeliwe tena au kama bado, basi usiangukie kwenye mtego huo, kuna mambo kadhaa ya kuzingatia wakati unapotaka kujihusisha na biashara mtandaoni.

1. Taarifa za kampuni
Endapo mhusika ana uza mavazi, magari au kitu kingine, hakikisha unapata taarifa za kina kuhusu kampuni hiyo ikiwemo jina halali, tovuti na mawasiliano mengine (sanduku la posta, anuani ya ofisi) ili kujiridhisha kama ni kampuni au duka halali.

Anapokupa namba za simu piga kujiridhisha au tovuti itembelee uone kama inaendana na kile anachokifanya. Endapo tovuti itakuwa na matangazo (click ads na pop-up ads), lugha isiyo rasmi au ‘link’ yake inaonekana sio salama, hiyo ni ishara kwamba unakaribia kupigwa.

Endapo jina la kampuni ni Swahili Times, ni wazi tovuti itakuwa www.swahilitimes.com au co.tz. Endapo utaona jina la kampuni halifanani na anuani ya tovuti, huenda huo ni wizi. Pia epuka kubonyeza kila ‘link’ inayotumwa kwako, kwani zinaweza kutumika kukutapeli.

2. Taarifa binafsi
Usimtumie mtu taarifa binafsi au kujisajili katika tovuti za biashara ambazo huna uhakika kama ni halali. Matapeli mitandao watatumia taarifa utakazowapa kukutapeli wewe, ndugu au marafiki zako. Toa taaarifa zako pale unapojiridhisha kwamba unayewasiliana naye ni mtu au taasisi halali.

Hakikia unakuwa na nywila imara kulinda taarifa zako.

3. Ushauri wa wengine
Njia nyingine ya kuepuka matapeli ni kuuliza marafiki au ndugu kuhusu mtu au kampuni ambayo unakusudia kununua kitu kutoka huko. Haiwezekani wewe ukawa ndio wa kwanza, hivyo kama yupo ambaye amenunua kitu kutoka kwa mtu au taasisi hiyo atakupa ushauri na utakuwa na uhakika.

Hapa pia unaweza kutumia ‘reviews’ za mtandaoni kuona wateja wengine wanasema nini kuhusu biashara husika.

4. Kutuma fedha
Ni wazi kuwa watu wengi wanafanya miamala mitandaoni, na lengo hapa sio kukwambia usitume fedha, bali fanya hivyo baada ya kujiridhisha kwamba unapotuma ni halali.

Endapo unayefanya naye biashara anakung’ang’aniza utume fedha kuliko anavyoeleza namna utakavyopata mzigo wako, unaweza kuanza kumtilia shaka. Utaratibu usio na mashaka ni ule wa mteja kulipa baada ya kupokea mzigo.

Lakini pia, endapo unapotuma fedha, jina la kampuni silo linaloonekana kwenye muamala, ni ishara nyingine ya kutia shaka. Epuka kutumia akaunti ya benki inayohifadhi fedha zako. Tumia njia mbadala kama PayPal au kutengeneza master card kupitia mitandao ya simu.

5. Mamlaka za biashara
Unaweza kupata taarifa zaidi kwa mamlaka zinazohusika na usajili wa biashara kuona kama kampuni husika inatambulika.

6. Fika kwenye taasisi
Kama uwezekano wa wewe mteja kufika kwenye duka au kampuni unapotaka kununua kitu upo, basi fanya hivyo kwani ni njia salama zaidi kuepuka kutapeliwa.

Hizi ni sehemu za njia hizo, unaweza kuongeza nyingine kwenye sanduku la maoni hapa chini au kwenye mitandao yetu ya kijamii ili kuwawezesha wengine wasitapeliwe.

 

Send this to a friend