NMB yaingia makubaliano kuwezesha mashirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi Zanzibar

0
36

Benki ya NMB imesaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Idara ya Mashirikiano baina ya Sekta za Serikali na Sekta Binafsi (PPP) iliyopo chini ya Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakaowezesha ufadhili wa miradi ya maendeleo na ya kimkakati visiwani humo.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo visiwani Zanzibar jana, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB Juma Kimori alisema makubaliano hayo ni mwendelezo wa mkakati wa benki hiyo unaolenga kujenga thamani ya pamoja kwa wadau wake wote ikiwemo Serikali na kusisitiza kuwa makubaliano hayo yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi visiwani Zanzibar.

“Makubaliano ambayo tumetia saini leo ni ya kimkakati na yatasaidia ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa lengo la kuimarisha maendeleo na uchumi wa Zanzibar. Sisi kama benki ya NMB tunatambua kuwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ndio njia rahisi itakayosaidia kukamilisha miradi mingi kwa haraka. Tunaamini pia kuwa bila ushirikiano na sekta binafsi hatuwezi kufikia uchumi wa bluu kwa kasi inavyotakiwa,” Kimori alisema.

Aliongeza kuwa makubailiano hayo yanalenga kuimarisha miundombinu ya uwekekezaji, ili kuwajengea mazingira mazuri wawekezaji wenye nia ya kuwekeza visiwani Zanzibar nakuongeza kuwa benki yake inaamini kwa ushirikiano huo utanufaisha maelfu ya wakazi wa Zanzibar kupitia miradi mbali mbali yenye chachu ya ukuaji wa uchumi.

Kimori alibainisha kuwa Benki ya NMB itatumia mizania yake madhubuti kutoa huduma za dhamana ya zabuni kwa wananchi na makampuni yanayotaka kushiriki katika miradi mbali mbali ya kimkakati ya maendeleo visiwani Zanzibar na kuongeza kuwa benki hiyo inatoa bidha za kipekee kwa wateja wake zinazowawezesha kushiriki kikamilifu.

“Benki yetu kwa miaka mingi sasa imekuwa ikiongoza katika suala la faida na nikiri kuwa kwa sasa tuna mizania thabiti. Kutokana na mizania yetu tunatoa hadi shilingi milioni 420 kwa mkupuo kwa mkopaji mmoja ambaye anakidhi vigezo na masharti yetu,” alisisitiza.

Kimori aliongeza kuwa benki hiyo inaendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali visiwani Zanzibar zikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ) huku akisistiza kuwa benki yake na itaendelea kufanya kazi na taasisi mbalimbali katika kufanikisha azma ya Zanzibar ya uchumi wa bluu.

Alibainisha kuwa benki hiyo itaendelea kutoa elimu ya kifedha na kubainisha kuwa zaidi ya watu 10,000 kutoka visiwani Zanzibar wanaojishughulisha na kilimo cha mwani, chumvi na tayari wamenufaika na mpango huo.

“Tunaimani kuimarika kwa uwekezaji Zanzibar kutasaidia kutoa fursa kwa vijana kupata ajira na serikali kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla,” Kimori aliongeza.

Naye Dk. Bill Kiwia, Kamishna wa Ukuzaji Uchumi na Miradi ya Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) wakati wa hafla hiyo alisema makubaliano hayo ni ya kihostoria na kipekee huku akiongeza kuwa yatakuwa chachu ya maendeleo visiwani Zanzibar kuanzia ngazi za chini.

“Makubaliano haya ni ya kihistoria kwa kuwa yanabainisha kuwa sekta ya Umma na binafsi zinaweza kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya wananchi kwa jumla. Nimatumaini yangu kuwa miradi itakayotelelezwa kupitia makubaliano haya italeta ahueni kubwa kwa wananchi kuanzia ngazi za chini,” alisema.

Naye Mudrik Ramadhan Soraga,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar wakati wa hafla hiyo aliipongeza benki ya NMB kwa kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Zanzibar huku akisema benki hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo visiwani Zanzibar.

Soraga alisema Serikali yake chini ya Dkt. Hussein Mwinyi inaamini katika kushirikiano na sekta binafsi katika kukuza maendeleo visiwani Zanzibar na kusisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na sekta binafsi pale ambapo kuna tija na pale ambapo kuna mapungufu.


“Tumeanza mchakato wa kubainisha miradi ya kati ambapo tutashirikiana na sekta binafsi kuitekeleza. Miradi hii lazima iwe imekubalika na jamii husika na lazima iwe na lengo la kutatua changamoto zinazoikabili jamii,” alisema

Send this to a friend