NMB yapata heshima kubwa ya Superbrands

0
51

Benki ya NMB imetunukiwa cheti cha kuwa ‘Superbrand’, na kuifanya kuwa benki pekee iliyopata hadhi hiyo nchini Tanzania mwaka huu.

Hadhi hiyo ya ‘Superbrands’ inatunukiwa chapa bora zaidi katika uwanja wao kufuatia mchakato mkali wa uteuzi na baraza la Superbrands na watumiaji wa bidhaa na huduma kutoka kote Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea cheti hicho iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mweka Hazina wa NMB, Aziz Chacha alisema hadhi ya Superbrands ina maana kubwa kwa benki hiyo na kusisitiza kuwa cheti hicho ni chachu ya kuifanya benki yake kuwa chaguo kwa wateja wake.

“Hili lisingewezekana bila imani iliyopo kwa wateja wetu ambao wamekuwa bega kwa bega nasi kwa miaka hii yote. Kama benki, tunafurahi kwamba wateja wetu wameweza kuamini chapa yetu na kuifanya kuwa miongoni mwa chapa bora Afrika Mashariki,” alisema.

Alibainisha kuwa benki hiyo imejipanga kuendelea kuongeza thamani kwa wadau wake wote wakiwemo wanahisa, wateja na jamii ambako benki hiyo inafanya kazi.

Alizishukuru mamlaka zote za udhibiti zikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kufanya kazi kwa karibu na benki hiyo na kusisitiza kuwa miongozo ya mamlaka hizo imesaidia kujenga misingi imara kwa benki yake.

Awali, Jawad Jaffer Mkurugenzi wa Mradi wa Superbrands na Mchapishaji alisema kufikia hadhi ya Superbrands huimarisha nafasi ya chapa, huongeza heshima na kuwahakikishia watumiaji na wasambazaji kwamba wananunua chapa bora zaidi.

“Hadhi ya Superbrand inazipa faida kubwa kwa wanaoipata, inaongeza heshima kwa kampuni dhidi ya washindani wake na inadhihiririsha kuwa mlaji wa mwisho anapata bidha bora kabisa,” alibainisha.

“Kupokea hadhi ya Superbrand ni jambo moja. Kuitunza ni jambo lingine. Nachukua wakati huu kukumbusha kampuni zote ambazo zimepokea hadhi hii leo kufanya juu chini ili kuhakikisha kwamba zinaidumisha,” alisisitiza.

Alisema kampuni zote tano zilizopokea hadhi ya Superbrand zitatunukiwa tuzo wakati wa sherehe zilizopangwa kufanyika mwaka kesho.

Send this to a friend