Nyumba 50 kwenye jengo la Uhuru Heights kuuzwa

0
41

Kampuni ya Cosmos Properties ya jijini Dar es Salaam, ambayo ni mmiliki wa nyumba 50 katika jengo la Uhuru Heights iko matatani baada ya nyumba hizo kutolewa notisi ya kuuzwa ili kufidia deni linalotokana na mkopo wa Benki ya Exim.

Mdaiwa huyo aligomea kuiruhusu kampuni ya uwakili ya Hallmark Attorneys iliyopewa nguvu ya kisheria na benki hiyo kusimamia mali hizo kutekeleza agizo hilo.

Tukio la mdaiwa huyo kugomea uamuzi huo wa kisheria limetokea mwanzoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam mara baada ya maofisa wa kampuni ya uwakili ya Hallmark Attorneys kufika kwenye jengo la Uhuru Heights kufanya ukaguzi wa kutathmini mali hizo, ambapo licha ya mdaiwa huyo kuonyeshwa nyaraka zote muhimu ikiwemo hati ya taarifa ya utekelezaji wa amri bado aligoma kutii agizo hilo.

Akizugumzia tukio hilo, Walter Chipeta ambae ni mshirika wa kampuni ya uwakili ya Hallmark Attorneys amesema kufuatia kitendo kilichofanywa na mdeni huyo, kampuni yake imejipanga kuendelea na mkakati wake wa kuhakikisha inafanikiwa kuzipata mali hizo licha ya ukinzania mkubwa kutoka kwa mdeni huyo.

“Hivi hapa tunapoongea tayari tunaendelea na hatua kisheria ambapo pamoja na mambo mengine tayari tumeripoti tukio hilo kwa jeshi la Polisi kwa kuwa mdeni huyu si tu kwamba alituzuia kufanya kazi yetu bali pia alisababisha vurugu ambazo zilitishia usalama wa baadhi ya maofisa wetu,” amesema Chipeta.

Hata hivyo alipotafutwa kwa njia ya simu Owais Pardesi ambaye ndio Mwenyekiti na mmiliki wa kampuni ya Cosmos Properties hakupatikana kwa njia ya simu na huku pia jitihada za kumtafuta zikiendelea.

Send this to a friend