Nyumba ya Askari Polisi yachomwa moto na wasiojulikana Songwe

0
117

Watu wasiojulikana wameteketeza kwa moto nyumba ya Mkaguzi wa Polisi Nsajigwa Mwajeka, ambaye ni Polisi Kata wa Kata ya Chitete, Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, na kusababisha hasara ya mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 2.

Akizungumza leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga amesema tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 22, 2025, wakati askari huyo alikuwa akitekeleza majukumu maalumu nje ya makazi yake.

Moto huo, ulioteketeza vyumba viwili vya nyumba hiyo, uligunduliwa na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chitete, Darkson Kamendu, ambaye alitoa taarifa kwa mamlaka husika.

Baadhi ya mali zilizoharibiwa ni nguo za kiraia, sare za polisi, vyombo vya nyumbani, mahindi, kitanda, godoro na vifaa vingine vya matumizi ya nyumbani.

Kamanda Senga amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wahalifu walikusanya vitu ndani ya nyumba na kuvichoma kwa kutumia njiti za kiberiti, ambazo zilipatikana eneo la tukio.

“Chanzo kamili bado kinachunguzwa, lakini inaonekana moto huo ulipangwa kwa makusudi,” alisema Kamanda Senga.

Hadi sasa hakuna mtuhumiwa aliyekamatwa, lakini Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua kali za kisheria mara watakapotiwa mbaroni.

Send this to a friend