Odinga aiomba radhi Rwanda kwa niaba ya serikali ya Kenya

0
20

Kiongozi wa Muungano wa Azimio La Umoja Kenya, Raila Odinga amelaani matamshi tata yaliyotolewa na Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, Kipchumba Murkomen ambayo yameonekana kukosoa utawala wa Rwanda.

Akiongea kwenye kipindi cha Monday Report cha Citizen TV, Murkomen alisema Kenya haifai kulinganishwa na Rwanda kimaendeleo, akisema kuwa wakati Nairobi ni taifa la kidemokrasia, Kigali ni nchi ya kiimla ambapo chochote anachosema Rais ni sheria.

Katika taarifa yake, Odinga ameyataja maneno ya Murkomen kuwa ya kusikitisha, yasiyo na staha na yasiyokuwa ya diplomasia dhidi ya Rwanda, huku akipinga kauli yake kuwa Rwanda ni nchi ndogo inayolinganishwa na kaunti ya Kajiado ya nchini Kenya.

“Jana tuliibua vita nyingine na Rwanda kupitia waziri wa barabara kwa kutumia lugha isiyo na staha na isiyokuwa na diplomasia dhidi ya nchi jirani mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Uanadiplomasia unahitaji mwenendo tofauti zaidi ya saa ghali, suti na fimbo za kutembelea,” amesema Odinga.

Ameongeza, “lugha ya kashfa iliyotumika dhidi ya nchi kubwa na watu wa Rwanda ni ya kusikitisha zaidi. Rwanda ni sawa na Uswisi na ukubwa wake ni mkubwa kuliko Singapore. Sio ukubwa unaofanya mataifa bali ni maono na uongozi. Kwa ndugu na dada zetu wa Rwanda, tunawaomba msamaha kwa dhambi za utawala uliolewa na nguvu na ufisadi.”

Send this to a friend