Odinga alaani kauli ya Ruto ya kuwaruhusu askari kuwapiga risasi raia

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amelaani vikali agizo lililotolewa hivi karibuni na Rais William Ruto la kuwaruhusu maafisa wa polisi kuwapiga risasi raia wanaoshiriki katika uporaji wa mali wakati wa maandamano, akisema hatua hiyo ni kinyume na Katiba na misingi ya haki za binadamu.
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Raila amesema kuwa hakuna hali yoyote ya maandamano au usimamizi wa sheria inayostahili amri ya kupiga risasi kwa lengo la kuua, kulemaza au kutisha raia.
“Maagizo kama hayo ni makosa kikatiba na ni hatari kwa taifa letu,” amesema Raila. “Kama taifa tunapaswa kusimama kwenye msingi wa utawala wa sheria na kuheshimu mchakato wa haki.”
Amesema kutoa mamlaka ya kutumia nguvu kwa polisi dhidi ya raia wanaoshukiwa kufanya makosa kunakiuka haki ya msingi ya mtu kuwa hana hatia hadi atakapothibitishwa na mahakama.
Katika taarifa hiyo, Raila ameisihi serikali na vyombo vya usalama kuweka mkazo kwenye kuwakamata watuhumiwa kwa mujibu wa sheria na kuwaweka kizimbani, badala ya kutumia nguvu au silaha za maangamizi.
“Tuchague kuwakamata na kuwaweka mahakamani badala ya kuwaua au kuwadhuru watuhumiwa. Hii siyo tu inalinda haki za binadamu, bali pia huipa serikali uhalali na uadilifu,” amesema.








