Odinga: Hatutakubali mtu mmoja kubadilisha yale ambayo Wakenya wameamua

0
23

 

Aliyekuwa mgombea urais kupitia tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga amepinga matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa Agosti 15, 2022 na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati ambapo William Ruto alitangazwa kuwa mshindi.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kupitia vyombo vya habari, Odinga amesema Chebukati amepindua matokeo na kutengana na wenzake, hivyo hawatakubali mtu mmoja abadilisha kile ambacho Wakenya wameamua.

Ruto: Sitokuwa na kisasi na mtu yeyote

“Hatutakubali mtu mmoja ajaribu kuleta vurugu katika taifa letu, kujaribu kubadilisha yale ambayo wameamua watu wa Kenya, hatutakubali. Tutazidi kuitetea nchi yetu na katiba yetu kama Wakenya, ili Kenya iweze kuendelea mbele,” amesema Odinga.

Mbali na hayo, Odinga amewashukuru Wakenya walioshiriki uchaguzi pamoja na wafuasi wa AZIMIO kwa kutofanya fujo au kujichukulia hatua mkononi baada ya matokeo kutangazwa na kuwaomba waendelee kuwa watulivu.

Aidha, Makamishna wanne wa Tume ya Uchaguzi wakiongozwa na Makamu mwenyekiti, Juliana Cherera wametoa sababu za kutokubaliana na matokeo hayo wakidai hesabu ya mwisho ya matokeo haikuletwa mbele ya tume ili kushughulikiwa.

Wameongeza kuwa ujumlishaji wa matokeo haukuwa sahihi kimahesabu, na kwamba matokeo hayo hayajumuishi jumla ya waliojiandikisha kupiga kura na kura zilizopigwa au zilizokataliwa, huku wakidai Mwenyekiti Chebukati aliwapindua na kusisitiza kutangaza matokeo licha ya wasiwasi wao.

 

Send this to a friend