
Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, amedai kuwa ameshinda karibu chaguzi zote za urais alizogombea, lakini hakuwahi kutangazwa rasmi kuwa mshindi akisema uchaguzi pekee wa huru na haki uliowahi kufanyika Kenya ulikuwa wa mwaka 2002.
Kauli yake imekuja wakati akimjibu Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu, ambaye alimshauri kushirikiana na Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka kuelekea uchaguzi wa 2027 ili kumshinda Rais William Ruto.
Odinga amewataka wanaomsukuma kugombea kwa mara ya sita watulie, akisema kuwa wakati wa uchaguzi utafika. Pia ameonya kuwa siasa zisipoendeshwa kwa tahadhari, zinaweza kuleta mgawanyiko mkubwa nchini.
Odinga, ambaye hivi karibuni amesaini mkataba wa ushirikiano wa kisiasa na Rais William Ruto, amesema kuwa taifa linapaswa kuungana ili kushughulikia changamoto zinazolikumba badala ya kumlazimisha Rais aondoke madarakani.