Onyo la serikali kwa wamiliki wa vituo vya kulea watoto yatima
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya baadhi ya wamiliki na waendeshaji wa makao ya watoto wasiofuata taratibu za usajili wa watoto, wanaowatumia watoto kama mitaji au kwa maslahi binafsi na wanaoendesha makao hayo kwa minajili ya kidini na kikabila.
Amewataka pia wamiliki hao waache mara moja kuwalea watoto hao katika maadili yasiyofaa na yasiyo ya Kitanzania na kwamba maofisa ustawi wa jamii wahusike moja kwa moja katika usajili wa mtoto ili kuhakikisha kuwa ni watoto wanaostahili tu kuwekwa kwenye makao ndiyo wanasajiliwa.
Alikuwa akizungumza jana usiku (Jumapili, Mei 26, 2019) kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam alikokuwa mgeni wa heshima wakati wa futari ya pamoja na watoto yatima kutoka kwenye vituo sita vya kulea watoto yatima vya jijini humo.
“Nitoe rai kwamba watu mmoja mmoja, taasisi na makao wazingatie baadhi ya taratibu za msingi za uendeshaji wa makao kama vile mtoto kukuzwa katika mazingira ya familia, kuzingatia misingi ya kitaifa badala ya misingi ya tamaduni za kigeni.
“Mtoto kukuzwa kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto; kuzingatia umuhimu wa kuwa na mwendelezo katika dini ya mtoto na utamuduni wake; kutotenganisha watoto na ndugu na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma stahiki, kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji; na kutunzwa na kuendelezwa hadi kufikia kimo cha utimilifu wao,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia hadhara hiyo pia kutoa maelekezo mahsusi kwa waendeshaji wa makao pamoja na wasimamizi wa sheria na taratibu za uendeshaji wa makao ya watoto yatima.
“Afisa Ustawi wa Jamii katika eneo yanakoanzishwa makao, ahusike moja kwa moja katika usajili wa mtoto ili kuhakikisha kuwa ni watoto wanaostahili tu kuwekwa kwenye makao ndio wanasajiliwa.
“Taasisi na makao zihakikishe kuwa kila mtoto anawekewa mpango maalumu wa kuondoka kwenye makao na namna ya kumuunganisha mtoto huyo na familia yake.
“Wamiliki wa taasisi na makao, waruhusuni maafisa ustawi wa jamii na maafisa wengine wa Serikali wafanye ukaguzi kwa mujibu wa sheria na wekeni utaratibu wa kuandaa taarifa za kila mwezi za watoto na taarifa ya mwaka wa fedha,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu pia alionya dhidi ya wale “wanaowabadili watoto dini kinyume cha sheria; wanaofanya vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto; wasiowaruhusu watendaji wa Serikali kufanya ufuatiliaji na usimamizi; wasioandaa mpango wa kuwaunganisha watoto na familia zao na hivyo, kusababisha watoto kukaa kwa muda mrefu kwenye makao na wale wote wanaondesha makao bila kuwa na leseni ya uendeshaji.”
Alisema Serikali haitowafumbia macho watu wa namna hiyo, na mara tu watakapogundulika kuanzisha au kuendesha makao bila kufuata taratibu, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema tangu mwaka 2016 hadi sasa, kuna jumla ya watoto 24,067 wanaolelewa katika makao yaliyosajiliwa nchini yakiwemo makao 140 yanayoendeshwa na kumilikiwa na watu au taasisi binafsi. Kati yao wavulana ni 11,925 na wasichana ni 12,142.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaratibu upatikanaji wa huduma za msingi kwenye makao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Baadhi ya huduma hizo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa Bima ya Afya kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. “Hadi sasa, watoto 900 kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha wamepatiwa kadi hizo na zoezi hilo linaendelea,” alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu uendeshaji wa makao ya watoto sambamba na kutoa elimu kuhusu malezi, makuzi, haki, ulinzi na usalama wa mtoto kwa mujibu wa sheria zinazosimamia haki na ustawi wa mtoto.
Mapema, akielezea azma ya kuandaa futari hiyo, Mkurugenzi wa Chocolate Princess na mwandaaji wa kipindi cha televisheni maarufu cha The Mboni Talk Show, Bi. Mboni Masimba alisema jumla ya watoto yatima 325 walikuwa wamealikwa kushiriki futari hiyo.
Watoto hao wanatoka vituo vya Ijango Zaida Orphanage Centre kilichopo Sinza, Alzama Orphanage Centre (Mbagala), Ashura Foundation (Vingunguti), Madina Orphanage Centre (Tandale), Hiyari Orphanage Centre (Mbagala) na Hisani Orphanage Centre (Mwasonga).
Futari hiyo iliandaliwa na Mboni Masimba kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Asure Yetim Vafki, United Bank of Africa (UBA), Junaco, Mo Dewji Foundation, Lake Oil, ASAS, AZAM, Uncle K Catering, Zurii, Simply Special Decor na State Oil na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo Balozi wa Uturuki nchini, Bw. Ali Davutoğlu, Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Issa Othman, masheikh, maimamu wa misikiti na viongozi wa taasisi zinazojihusisha na malezi ya watoto yatima.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,