Orodha ya majimbo ambayo NEC imerejesha wagombea waliowekewa zuio
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekubali rufaa 13 na imewarejesha katika orodha ya wagombea Ubunge wagombea 13 baada ya kupitia nyaraka walizowasilisha.
Rufaa hizo ni kutoka majimbo ya Singida Magharibi, Madaba, Ilemela, Namtumbo, Bagamoyo, Liwale, Tunduma, Bukene na Kigamboni.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Charles Mahera ambapo amesema kuwa wametoa uamuzi wa rufaa 34 za wagombea ubunge.
Aidha, NEC imekataa rufaa 7 za wagombea ambao hawakuteuliwa kutoka majimbo ya Singida Magharibi, Bahi, Handeni Vijijini, Madaba, Singida Mashariki, Ileje, Meatu na Bukene.
Pia, NEC imekataa rufaa 14 za kupinga walioteuliwa ambapo rufaa hizo ziliwasilishwa kutoka majimbo ya Mwanga, Mafinga, Ilala, Manonga, Iguga na Kisesa.
Hadi sasa rufaa zilizofanyiwa kazi na tume ni 89, ambapo Septemba 8 mwaka huu taasisi hiyo ilitoa uamuzi wa rufaa 55.
Mahera amesema kuwa tume imechambua vielelezo, nyaraka na maelezo ya warufani na warufaniwa vilivyowasilishwa ili kuhakikisha inatenda haki wa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Tume imeongeza kuwa itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo.