Orodha ya Marais 10 wa Afrika wenye umri mkubwa zaidi

0
20

Bola Tinubu (70) amechaguliwa kuwa Rais wa Nigeria akitarajiwa kuchukua nafasi ya Muhammadu Buhari.

Kufuatia ushindi huo, mjadala mkubwa umeibuka kupitia mitandao ya kijamii, wachangiaji wengi wakikosoa Taifa hilo kuchagua kiongozi mwenye umri mkubwa.

Lakini kikubwa cha kufahamu ni kuwa bara la Afrika si nyumbani kwa Marais wenye umri mkubwa pekee duniani, bali hata viongozi ambao wameshika madaraka kwa muda mrefu zaidi.

Hawa baadhi yao;

1. Paul Biya (89), Rais wa Cameroon
Alizaliwa mwaka 1933 na kutawala Cameroon tangu 1982. Anashika nafasi ya pili katika orodha ya Marais waliohudumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika, na Mkuu wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani.

Biya ni maarufu kwa kubadilisha sheria ili kupanua utawala wake. Amekuwa madarakani kwa miongo minne na anatarajiwa kusalia madarakani hadi 2025 wakati muda wake utakapomalizika.

2. Hage Gottfried Geingob (81), Rais wa Namibia
Alichaguliwa mwaka 2014 na kuwa Rais wa tatu wa Namibia. Rais huyu amekuwa madarakani kwa miaka nane. Katiba ya Namibia inaeleza kuwa kikomo cha muhula wa Rais ni miaka mitano.

3. Alassane Dramane Ouattara (80), Rais wa Ivory Coast
Alishika wadhifa kama Rais wa tano wa Ivory Coast mnamo 2010, na amekuwa madarakani kwa miaka 12. Katiba ya nchi inasema mgombea urais awe na umri kati ya miaka 35 hadi 70.

4. Teodoro Nguema Mbasogo (80), Rais wa Guinea ya Ikweta
Alizaliwa mwaka 1942, Rais Mbasogo amekuwa madarakani tangu 1979 akitimiza miaka 43 kama mkuu wa nchi hiyo huku akiongoza kwa kukaa madarakani kwa muda mrefu kuliko nchi yoyote ile, na kiongozi wa pili kwa kuongoza taifa kwa sasa asiye wa kifalme duniani kwa muda mrefu mfululizo.

5. Emmerson Mnangagwa (80), Rais wa Zimbabwe
Rais wa Zimbabwe aliingia madarakani mwaka 2017, na kuna uwezekano atakuwapo kwa muda zaidi ukizingatia katiba ya nchi inamruhusu kuhudumu kwa mihula miwili hadi mitano.

Alikuwa mshirika wa muda mrefu wa hayati Rais Robert Mugabe, Mnangagwa pia aliwahi kuwa Makamu wa Rais Mugabe hadi Novemba 2017.

6. Muhammadu Buhari (80), Rais wa Nigeria
Alizaliwa mwaka 1942. Rais Buhari amekuwa mkuu wa nchi wa Nigeria tangu 2015 akiwa amehudumu kwa miaka 7. Buhari aliwahakikishia Wanigeria kwamba hatabadilisha katiba ili kuongeza ukomo wa muhula wake.

7. Nana Akufo-Addo (78), Rais wa Ghana
Rais Akufo- Addo alishika wadhifa huo mwaka 2017, aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2008 na 2012 lakini akashindwa.

Nchini Ghana, Rais amewekewa mihula miwili pekee huku uchaguzi ukifanyika baada ya miaka minne.

8. Yoweri Museveni (78), Rais wa Uganda
Rais huyu wa Uganda mwenye umri wa miaka 78 ndiye Rais wa Afrika Mashariki aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi akihudumu kwa miaka 36 baada ya kunufaika mara mbili na mabadiliko ya katiba.

Wabunge wa Uganda mwaka 2005 waliondoa ukomo wa mihula inayomruhusu Rais Museveni kusalia madarakani, na mwaka wa 2017 wabunge hao tena walipiga kura kwa wingi kufuta ukomo wa umri wa miaka 75 kwa wagombea urais, na kumruhusu Museveni kuwania kwa mara nyingine tena.

9. Abdelmadjid Tebboune (76), Rais wa Algeria
Alizaliwa mwaka 1945, akaingia madarakani mwaka 2019. Mzee huyo mwenye umri wa miaka 76 alilazwa nchini Ujerumani kwa miezi miwili kufuatia kuripotiwa visa vya UVIKO-19 miongoni mwa wafanyikazi wake.

Katika mageuzi ya hivi majuzi ya katiba, Waalgeria walipiga kura ya kuweka ukomo wa mihula ya Rais kwa miaka miwili hadi mitano madarakani.

10. Ismail Omar Guelleh (74), Rais wa Djibouti
Rais Guelleh ametawala Djibouti kwa miaka 23 tangu mwaka 1999 na kumfanya kuwa mmoja wa watawala waliohudumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.