P-Square waungana baada ya kumaliza tofauti zao

0
49

Wanamuziki mapacha waliokuwa wakiunda kundi la P-Square, moja kati ya kundi bora la Afrobeats, wamemaliza tofauti zao, baada ya kutofautiana kwa miaka kadhaa.

Wasanii hao kutoka Nigeria Peter na Paul Okoye walivunja muungano huo mwaka 2017 kufuatia mgogoro wa kifamilia

Leo wamesherehekea mwaka wa 40 tangu kuzaliwa kwao huku wakiwajuza mashabiki wao kuwa wamemaliza kilichokuwa kikiwatenganisha.

Hata hivyo hawajaweka wazi endapo watarudisha kundi lao na kufanya nyimbo pamoja. Hata hivyo mashabiki wametamani kuwaona wakali hao wa nyimbo kama Do Me, Tempitation, Chop My Money na Bizzybody, wakifanya tena kazi pamoja.

Sababu hasa iliyowatenganisha haikuwahi kuwekwa wazi, hata hivyo huko nyuma jitihada za kuwasuluhisha kutoka kwa wanasiasa, viongozi wa dini na watu mashuhuri ziligonga mwamba.

Hata hivyo tetesi zinadai kuwa kuvunjika kwao kuliwahusisha wake zao na kaka yao ambaye pia alikuwa meneja wao.

Kupitia ukurasa wa Instagram wameandika “Vichwa 2 ni nora kuliko kimoja.”

Baada ya P-Square kuvunjika, kila mmoja alitumia jina tofauti ambapo Peter alijiita Mr. P na Paul akitambulika kama Rudeboy, lakini hakuna aliyefikia mafanikio yao wakiwa kama P-Square.

Send this to a friend