Padri adaiwa kubaka, kulawiti watoto zaidi ya 10

0
42

Padri mmoja wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi anadaiwa kushikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwabaka na kuwalawiti watoto zaidi ya 10, ambao ni wanafunzi kuanzia darasa la sita hadi kidato cha kwanza waliokuwa wakihudhuria katika mafundisho ya komunio ya kwanza na kipaimara.

Inadaiwa, Padri huyo kila alipomaliza haja zake, aliwapa kila mmoja kati ya Shilingi 3, 000 na Shilingi 5,000.

Wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, akikataa kuthibitisha au kukanusha kukamatwa kwa padri huyo, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu amethibitisha uwepo wa tukio hilo na kulaani kuwa “ni baya linalofedhehesha”.

“Katika tabia mbaya zisizo za watu waliostaarabika ni hizo, inaonekana mkoa wetu umezidi kuwa na matukio kama haya. Naviagiza vyombo vya usalama kwamba mtu yeyote atakayekamatwa na ushahidi upo hakuna kurudi nyuma,” amesema RC Babu.

Atakayebadilisha, kufichua taarifa binafsi faini milioni 10

Tukio hilo ambalo ni la kwanza kusikika likifanywa na kiongozi wa dini mkoani Kilimanjaro, huku likihusisha idadi kubwa ya wanafunzi, limeibua taharuki kwa wazazi ambao walipanga kuandamana kwenda kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi katika Siku ya Amani Duniani ambayo kitaifa ilifanyika mjini Moshi, ili kupaza sauti zao kutokana na kigugumizi cha kukamatwa kwa padri huyo.

Inadaiwa baada ya polisi kupata fununu za wazazi kujipanga kuandamana na mabango kwenda kwa Waziri Mkuu, ndipo jioni ya Septemba 20, siku moja kabla ya kiongozi huyo kuwasili mkoani Kilimanjaro, walikwenda kumkamata.

Chanzo: Mwananchi.

Send this to a friend