Panya mtegua mabomu wa Tanzania astaafu na miaka 7

0
33

Magawa, panya kutoka Tanzania ambaye kwa miaka amekuwa akitumia kutegua mabomu/vilipuzi ya ardhini nchini Cambodia amestaafu akiwa na miaka 7.

Magawa ambaye alizaliwa Novemba 5, 2014 alikuwa mmoja wa panya mashukuru katika kunusa na kutambua mabomu ya ardhini ambapo mwaka 2020 alitunukiwa medali ya dhahabu kwa ujasiri wake wa kuokoa maisha na kujituma katika kazi (Lifesaving Bravery and Devotion to Duty).

Kwa kustaafu kwake, sasa ataishi akila ndizi mbivu na ‘peanut’, vyakula ambavyo alivipenda sana, na alikuwa akizawadiwa kila alipofanya vizuri kwenye kazi.

Panya huyo alifunzwa mkoani Morogoro na taasisi ya Apopo, ambapo katika miaka yake mitano ya kazi amesafisha eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 225,000, sawa na viwanja vya mpira wa miguu 42.

Katika miaka hiyo aliweza kubaini vilipuzi 71 na vitu visivyo vilipuzi 38, na mwajiri wake ameeleza kuwa sasa panya huyo amechoka hivyo amestaafu.

Magawa ana uwezo wa kusafisha eneo sawa na uwanja wa tenesi kwa dakika 30, zoezi ambalo lingetumia siku nne endapo njia ya kawaida ya kutambua vilipunzi ikitumika. Endapo atahisi kuna kilipuzi, Magawa humtaarifu msimamizi wake kwa kukwangua ardhi.

Mamilioni ya vilipuzi vilifukiwa ardhini nchini Cambodia kati ya mwaka 1975 na 1998 na vimekuwa vikisababisha athari kubwa kwenye maisha ya binadamu.