Panya road wapewa siku 7

0
76

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linawakamata vijana wa  kundi linalojihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu maarufu kama ‘panya road’.

Baada ya kufanya ziara katika Kata za Chanika na Zingiziwa hapo jana ili kusikiliza namna wananchi hao wanavyopata changamoto ya kuvamiwa na kundi hilo la uhalifu, Waziri Masauni ametoa agizo hilo na kusema hategemei kusikia malalamiko kuhusu kundi hilo.

“Hakikisheni vijana hao wote waliotenda uhalifu Chanika na Kunduchi  wanakamatwa ndani ya siku saba na sitegemei tena kuona raia yeyote wa Dar es salaam amekatwa panga.” amesema Waziri.

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amesema kuwa uchunguzi umebaini kuwa kundi hilo linaundwa na vijana 31 na kati yao 21 wanashikiliwa na Polisi.

Aidha Waziri Masuni amesema kuwa, Serikali imeajiri askari wapya 4,003 na kupandisha vyeo askari 27,000 ambao kati yao watapelekwa kufanya kazi Chanika kwa ajili ya kusaidiana na viongozi wa Serikali za Mitaa ili kuimarisha usalama.