Patrick Mgoya afungua kesi Mahakama Kuu kupinga ukomo wa Urais

0
15

Patrick Dezydelius Mgoya, mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam amefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania akihoji uhalali wa kifungu cha 40(2) cha katiba ya nchi, ambcho kinachotoa ukomo wa kipindi cha Urais.

Katika kesi hiyo, Mgoya ameomba mahakama kutoa ufafanuzi wa kina na athari za kifungu hicho cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia ameiomba mahakama kutoa ufafanuzi sahihi wa kisheria na wa kina wa kifungu cha 42(2) cha katiba, na namna kinavyohusiana na vifungu namba 13, 21 na 22.

Kifungu namba 13 kinazungumzia usawa mbele ya sheria, namba 21 kinaelezea uhuru wa kushiriki shughuli za umma huku namba 22 kikielezea haki ya kufanya kazi.

Ameomba mahakama kutoa ufafanuzi wa kifungu namba 40(2) kwa pamoja na kifungu namba 39 ambacho kinaelezea sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Rais.

Katika hoja yake Mgoya amesema kuwa kwa kuweka ukomo wa kipindi cha Urais, kifungu 40(20) kinakiuka vipengele vingine vya katiba ambavyo vinatoa uhuru kwa wanachi kushirki katika shunguli za umma.

Kesi ya Patrick imekuja kipindi ambacho Rais Dkt Magufuli amekuwa akisema mara kadhaa kwamba hana lengo la kubadilisha katiba ili aendelee kuwepo madarakani, na kwamba muda wake utakapomalizika, hatoongeza hata dakika tano kwani anaheshimu katiba ya nchi na chama.

Akizungumza na Maafisa Watendaji wa Kata Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Rais amesema kuwa kama ambavyo waliwepo viongozi wengine walioishi Ikulu na wakaondoka muda wao ulipokwisha, na yeye ataondoka muda ukiisha, na atakayekuja ataondoka pia.

“Ikulu ni kwa watanzania wote. Walikuwepo Wajerumani, wakaondoka, wakaja Waingereza, wakaondoka, wakaja Mwl. Nyerere, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa na Kikwete, wote wakaondoka, na mimi nitaondoka. Atakuja mwingine, na yeye ataondoka,” amesema Rais Dkt Magufuli

Send this to a friend