Petra Diamond yatangaza kuuza mgodi wa almasi uliopo Shinyanga

0
43

Kampuni ya kimataifa inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya almasi, Petra Diamonds imetangaza kuuza mgodi wake wa almasi uliopo nchini Tanzania.

Kampuni hiyo ambayo inamiliki Mgodi ya Williamson Diamond (Mine) uliopo 23KM Kaskazini Mashariki mwa mkoa wa Shinyanga pia imetangaza kuwa itauza migodi yake iliyopo nchini Afrika Kusini.

Akizungumza na Gazeti la The Citizen, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema kuwa serikali haijapewa taarifa rasmi kuhusu adhma hiyo.

“Hatuna taarifa ya taarifa ya uamuzi huo lakini tutafuatili,” amesema Nyongo akinukuliwa na gazeti hilo.

Serikali ya Tanzania inamiliki asilimia 25 ya Williamson Diamond Mine ambao mwaka 2017 ulikumbana na changamoto mbalimbali hasa baada ya Kamati ya Bunge la Tanzania kueleza kuwa mgodi huo umekuwa ukikwepa kodi.

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa mkataba ulioingiwa baina ya serikali na kampuni hiyo ulikuwa na kasoro mbalimbali, ambapo moja ya changamoto ni kutojulikana kwa kiasi halisi cha almasi ambacho kilikuwa kikisafirishwa kwenda nje ya nchi.

Mussa Zungu ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo alieleza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikipeleka nje ya nchi kiwango kikubwa cha madini, huku ikiidanganya serikali kuwa imekuwa ikipata hasara, lakini haikuacha kufanya kazi hiyo.

Taarifa za kifedha zinaonesha kuwa katika robo ya tatu ya mwaka iliyoishia Machi 31 mwaka huu mapato ya kampuni hiyo yalishuka kwa 32% kutokana na changamoto za kuuza zabuni zake ambako kuliathiriwa na janga la virusi vya corona.

Send this to a friend