Petroli inavyoathiri watoto wadogo wanaopakizwa kwenye bodaboda

0
20

Kupakia watoto chini ya umri wa miaka tisa kwenye pikipiki peke yao ni hatari inayozidi kuongezeka na inayozua wasiwasi kuhusu usalama wao barabarani. Hali hii inajitokeza katika maeneo mengi, hasa katika nchi zinazoendelea, ambapo usafiri wa pikipiki umekuwa ni usafiri wa haraka na rahisi zaidi katika majiji makubwa ikiwemo jiji la Dar es Salaam ambalo linakabiliwa na changamoto kubwa ya usafiri.

Watoto wadogo wanaotumia usafiri wa pikipiki na baadhi wakiwekwa mbele ya dereva, wanakutana na hatari kubwa ya ajali, majeraha, na hata vifo. Hali hii inachangiwa na ukosefu wa vifaa vya usalama kama vile kofia ngumu, lakini pia kukosa usawa wanapokuwa peke yao na kupelekea kuanguka kwa urahisi.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mratibu Mwandamizi wa Polisi, Solomon Mwangamilo, katika mahojiano na Swahili Times amesema watoto wadogo wanapokalishwa mbele ya dereva hukaa katika tenki la petroli ambapo kadiri pikipiki inapotikisa mtoto huvuta harufu ya petroli moja kwa moja lakini pia pindi ajali inapotekea mtu wa kwanza kuathirika ni mtoto huyo.

“Mtoto yule bado mapafu yake hayajakomaa kwa hiyo anavuta hewa ya moja kwa moja yenye vumbi, hewa nzito yenye moshi na kadhalika, anaweza akaathirika mapafu. Lakini athari hizi hatuzioni kwa leo, athari hizi zitaonekana miaka ya baadaye kwamba mtoto wangu amekuwa mkubwa mbona muda wote mapafu yanamsumbua kumbe msingi ulikuwa ni mbaya kwa wazazi,” amesema.

Akifafanua kuhusu adhabu, amesema bado hakuna sheria inayowaadabisha wazazi wanaoruhusu watoto chini ya miaka tisa kupakiwa kwenye pikipiki isipokuwa wanatoa elimu kwa jamii kuwalea watoto wao ipasavyo kwa kujali usalama wao.

Aidha, amesema adhabu ya dereva aliyepatikana na kosa hilo barabarani hutozwa faini ya shilingi 10,000 kwa kila kosa au kufikishwa mahakamani ikiwa kosa ni kubwa zaidi.

Send this to a friend