Polisi adaiwa kumjeruhi sehemu za siri mwanafunzi kwa tuhuma ya wizi wa ‘laptop’

0
33

Mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) kilichopo Mkoani Mwanza, Warren Lyimo anadaiwa kupigwa na kuvunjwa korodani na askari kutoka Jeshi la Polisi mkoani humo anayejulikana kwa jina la Fabian.

Inadaiwa askari huyo alitekeleza kitendo hico baada ya Lyimo kutuhumiwa kuiba kompyuta mpakato aina ya HP ENVY 360 Mei 16 mwaka huu na kupelekwa kituo kidogo cha Polisi Buhongwa.

Inasemekana, Askari alimshushia kipigo mwanachuo huyo kwa ngumi na mateke katika sehemu zake za mwili huku akitumia koleo kumkandamiza sehemu zake za siri akimlazimisha kukiri kosa hilo.

Ofisa Habari wa Hospitali ya Bugando, Jackline John amekiri kupokelewa kwa mwanachuo huyo akiwa na rufaa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana ‘Butimba’ na kulazwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Akizungumza na Raia Mwema baba mlezi wa kijana huyo, Frits Msajo amedai hakuwa na uhakika wa usalama wa kijana wake hospitalini hapo mara baada ya kumuona askari aliyemjeruhi eneo la hospitali akizunguka, hivyo aliongea na uongozi wa Polisi kisha kutolewa amri ya askari huyo kutoonekana eneo la hospitali.

“Madaktari nao walishangaa kumuona mtuhumiwa akizungunguka hospitalini hapo, ikabidi wamhamishie ICU kwa usalama wake na matibabu ya karibu. Nimewasiliana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camillius Wambura, pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini wamelaani tukio hilo na wameniahidi watalishughulikia” amedai.

Chanzo: Raia Mwema

Send this to a friend