
Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi wa video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha mwendesha pikipiki akikamatwa kwa nguvu na Polisi Februari 20, 2025 katika eneo la Maili Moja mkoani Pwani, ambapo limesema mtuhumiwa alikuwa anatafutwa kutokana na tuhuma mbalimbali za uporaji kwa kutumia pikipiki ikiwa imekunjwa namba za usajili na wakati mwingine haina kabisa.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema wakati mtuhumiwa huyo alipojaribu kuwakimbia Polisi walipojaribu kumkamata katika eneo la Mwendapole, pikipiki aliyokuwa anaendesha ilikuwa haina namba ya usajili.
“Wakati wa ukamataji alianzisha vurugu ili kukaidi ukamataji pamoja na Askari Polisi kujitambulisha kwake, hata hivyo walifanikiwa kumkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi Kibaha ili kuendelea na taratibu nyingine za kisheria kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa ndugu wa mtuhumiwa huyo wanazo taarifa kuwa anashikiliwa katika kituo hicho.