Polisi aliyetajwa na Rais Samia kwa kusifia gongo afukuzwa kazi

1
46

Konstebo wa Polisi, Ramadhani Khalfan Said amefukuzwa kazi kwa kwenda kinyume na mwenendo mema wa Jeshi la Polisi Tanzania baada ya kunaswa kwenye mkanda wa video akisifia pombe haramu aina ya gongo huku akiwa amevalia sare za jeshi hilo.

Imeelezwa kuwa kitendo hicho cha askari huyo aliyekuwa na namba G2308 kimelifedhehesha Jeshi la Polisi baada ya video hiyo kusambaa mitandaoni akisema kwamba Gongo ni pombe safi akiipa jina la NIPA (New International Pure Alcohol), video ambayo imeonwa na watu wengi akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.

“Yaani neno NIPA lina silabi nne. Maana yake ni kwamba ni New International Pure Alcohol, kwa maana ni kinywaji ambacho kiko safi na process  yake inayotumika ni ya kimaabara kabisa inaitwa distillation,” amesikika Said kwenye video hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema mbali na kosa hilo, Said alikuwa pia na makosa mengine ya utovu wa nidhamu.

Polisi wameeleza kwamba Oktoba 30 mwaka huu huko Kawawa Road, wilaya ya Moshi, kwa makusudi bila halali akiwa kazini kwenye sare za Jeshi la Polisi alimlaghai na kumchukua binti, mwanafunzi kidato cha tatu Shule ya Sekondari St. John Paul II na kumuingiza ndani ya gari lake (T.971 CVU Toyota Raum) kisha kuondoka nae. Baada ya muda alikutwa akiwa kwenye gari hilo huku amefunga milango akiwa amevua nguo zote kwa nia ya kufanya mapenzi na binti huyo. Askari huyo alifanikiwa kukimbia toka eneo la tukio akiwa na mwanafunzi huyo wakapata ajali na kuumia.

Uamuzi wa kumfukuza kazi ulifikiwa baada ya kufunguliwa mashitaka ya kijeshi na kutiwa hatiani.

Akifunga mafunzo ya kozi ya maofisa wa Jeshi la Polisi Desemba 12 mwaka huu mkoani Dar es Salaam, Rais Samia alizungumzia video hiyo na kuonesha kutoridhishwa na mwenendo wa askari huyo na kumuuliza IGP Simon Sirro kama ameiona, huku akikemea vitendo vya ukosefu wa maadili ndani ya jeshi.

 

Send this to a friend