Polisi Arusha watoa mitaji kwa warahibu wa dawa za kulevya

0
21

Mtandao wa Polisi Wanawake Mkoa wa Arusha wametoa mitaji kwa warahibu wa dawa za kulevya ambao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru.

Akiongea wakati wa kukabidhi mitaji hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa huo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, SSP Georgina Matagi amesema baada ya serikali kutoa huduma ya tiba kwa warahibu hao, wameona ni vyema kuunga juhudi hizo kwa kutoa mitaji ya biashara ili iweze kuwakwamua kiuchumi na kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

SSP Georgina ametaja baadhi ya misaada waliyoitoa kwa vikundi vya warahibu hao kuwa ni vifaa vya saluni ya kike na kodi ya pango ya saluni hiyo kwa muda wa miezi sita ambapo jumla imegharimu TZS 4,580,000, mtaji wa TZS 500,000 kwa ajili ya biashara ya matunda na mbogamboga, TZS 500,000 kwa ajili ya utengenezaji wa sabuni, na TZS 500,000 kwa ajili ya biashara ya mtumba.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Afya ya akili katika Hospitali hiyo ya Rufaa Dkt. Salum Seif amesema kituo hicho kilianza na jumla ya warahibu 12 ambapo mpaka sasa kinahudumia warahibu 746 ambapo wameona ni vyema kupitia siku 16 za kupinga ukatili kuwashirikisha wadau ikiwemo Jeshi la Polisi ili kulifikia kundi hilo ambalo ni wahanga wa ukatili wakisaikolojia na uchumi.

Akimwakilisha mganga mfadhiwi wa hosipitali hiyo Bi. Angel Kimati amewapongeza warahibu wa dawa za kulevya kwa uamuzi wao wa kufika katika kituo hicho na kupewa tiba huku akiwataka kutumia vyema mitaji waliyoipata kwenda kukuza vipato vyao.

Send this to a friend