Polisi: Bernard Morrison aache kujificha, afike kituo cha Polisi

0
4

Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi wa taarifa inayaosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mchezaji Bernard Morris kutuhumu huduma ya Kituo cha Polisi Mbweni.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema Machi 2024 Bernard Morrison alifungua kesi ya wizi kituo cha Polisi Mbweni ikidai akiwa Ghana alimtumia Abdul Rakeeb Mgaya kiasi cha TZS milioni 1 na laki 5 ili amkabidhi mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Boat anayeishi hapa nchini ili atafute timu itakayomsajili, lakini hafunya hivyo.

“Baada ya malalamiko hayo, mtuhumiwa alitafutwa na alipohojiwa alieleza ni kweli alitumiwa hizo fedha ili zisaidie kwenye gharama za kumsajili huyo mdogo wake lakini ilishindikana kwa sababu hakuwa na kiwango cha kusajiliwa na timu aliyokuwa anahitaji.

Hata hivyo, alimtaka Bernard Morrison ampe muda atamrejeshea fedha zake. Pia alielezwa kulingana na ushahidi, hakuna kesi ya jinai, hivyo walielewana na kwa vile wote ni raia wa Ghana walikubaliana kulipana,” imeeleza taarifa.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa, Juni 03, 2024 iliripotiwa kesi ya kuharibu mali, ambapo Bernard Morrison akiwa na mdogo wake na mtu mwingine, walifika katika nyumba anayoishi Abdul Rakeeb na kuvunja geti kisha kuchukua kwa nguvu gari aina ya IST namba T239 DFM.

Jeshi la Polisi limesema liliendelea kumtafuta Morrison bila mafanikio lakini walifanikiwa kuliona gari hilo likiwa limeegeshwa, kisha kulipeleka kituo cha Polisi Mbweni.

“Bernard Morrison anachotakiwa kufanya ni kuacha kujificha, kusema ukweli na kufikia kituo cha Polisi kuonana na uongozi ili sheria ichukue mkondo wake,” imesema.