Polisi: Gwajima afuate taratibu za kisheria badala ya kukaidi agizo la Msajili

0
6

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeutaka uongozi pamoja na waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, lililopo Ubungo mkoani Dar es Salaam, kuheshimu sheria baada ya kanisa hilo kufungiwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia.

Akizungumza katika kipindi cha Good Morning kinachorushwa na Wasafi Media, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema licha ya tamko rasmi kutolewa na msajili, kanisa hilo, ambalo kiongozi wake pia ni Mbunge wa Kawe, liliendelea kufanya ibada na shughuli zake kama kawaida, hali iliyolazimu Jeshi la Polisi kuwakamata baadhi ya waumini kwa ajili ya mahojiano.

“Wakati tunatoa maelekezo ya kisheria kuhusu nini cha kufanyika baada ya agizo la kufungwa kanisa hilo, baadhi ya watu walionekana kutofahamu au kupuuza maelekezo hayo. Hivyo, tuliwachukua kwa mahojiano ili kubaini kama walikuwa hawaelewi kweli au walikuwa wanakaidi kwa makusudi kwa nia ya kuchochea vurugu,” amesema Kamanda Muliro.

Aidha, amesisitiza kuwa iwapo Askofu Gwajima hajaridhishwa na hatua ya kufungiwa kwa kanisa lake, anatakiwa kufuata taratibu za kisheria zilizowekwa, ikiwemo kukata rufaa kwa mamlaka husika badala ya kukaidi maagizo ya serikali.

“Sisi kama Jeshi la Polisi tunatekeleza jukumu la kusimamia utekelezaji wa sheria. Kilichoelekezwa ni kusitisha shughuli za kanisa hilo, hivyo hazipaswi kuendelea hadi taratibu za kisheria zitakapokamilika. Kama Askofu anataka zirejee, basi afuate utaratibu wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kukata rufaa,” amefafanua.

Kamanda Muliro ameongeza kuwa Jeshi la Polisi limeweka alama na vizuizi katika eneo la kanisa hilo kuzuia shughuli kuendelea, na kwamba halitegemei kuwepo kwa mivutano kati ya waumini na vyombo vya usalama.

“Wananchi wengi wanajua kinachoendelea. Jeshi la Polisi lipo pale kuhakikisha amani na utekelezaji wa maagizo ya mamlaka. Hatutarajii kuwa na msuguano mkali kati yetu na waumini,” amesema.

Send this to a friend