Polisi: Hatutaruhusu uvunjifu wa amani mchezo wa Simba dhidi ya Stellenbosch

0
13

Kuelekea mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini utakaochezwa Aprili 20, 2025 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar,  Jeshi la Polisi limesema litahakikisha ulinzi unaimarishwa kipindi chote, wakati na baada ya mchezo huo.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ACP Abubakar Ally imesema haitamruhusu yeyote kufanya vitendo vyenye kuleta uvunjifu wa amani kwa namna yoyote.

“Tutahakikisha kwamba wananchi, wanachama, mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu wanashiriki katika mchezo huo kwa usalama na amani,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, imesema pamoja na kuwepo kwa mchezo huo, siku hiyo pia waumini wa dini ya Kikristo wanasherehekea Sikukuu ya Pasaka, hivyo Jeshi la Polisi litaimarisha ulinzi kuanzia mkesha wa Sikukuu katika nyumba za ibada na maeneo mbalimbali.