Polisi: Kada wa CHADEMA Mwanza aliuawa na wananchi wenye hasira

2
81

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema kuwa uchunguzi umebaini kwamba aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA Kata ya Buswelu, Erasto Makaranga alishambuliwa na wananchi wenye hasira hadi kufariki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng’anzi katika mahojiano na gazeti la Mwananchi amesema wananchi walimtuhumu kada huyo kuvunja na kuingia kwenye hosteli za nje za wanafunzi wa Chuo cha Biashara (CBE).

Makaranga alidaiwa kutoweka nyumbani kwake Novemba 7 mwaka huu kabla ya mwili wake kukutwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure siku 13 baadaye.

Kamanda Ng’anzi amesema wanafunzi wa hosteli hiyo walimpigia kelele za mwizi ndipo wananchi wakamshambulia na kusababisha kifo chake.

“Niwatake wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi wananpomtuhumu mtu kufanya uhalifu, na badala yake watoe taarifa polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake,” amesema kamanda huyo akizungumza na Mwananchi.

Hata hivyo familia ya marehemu imesema kifo cha ndugu yao kinahusishwa na masuala ya kisiasa, na hivyo kuliomba jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina.

 

Send this to a friend