Polisi kumsaka dereva aliyegonga na kuua watu 11 waliokuwa wakiangalia ajali Tanga
Jeshi la Polisi mkoani Tanga linamsaka dereva anayejulikana kwa jina la Baraka Merkizedek aliyekuwa akiendesha gari namba T.782 BTU aina ya Volvo baada ya kugonga watu waliokuwa pembeni mwa barabara wakiangalia ajali iliyokuwa imetokea eneo la Chang’ombe, Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni, baada gari aina ya TATA, basi lililokuwa limeteleza na kuacha barabara bila kusababisha madhara yoyote kwa binadamu.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imesema dereva huyo aliwagonga watu hao Januari 13, 2025, majira ya saa 3 usiku na kusababisha vifo vya watu kumi na moja na majeruhi kumi na wawili.
Waliofariki na kutambuliwa katika ajali hiyo mi Hamis maarufu kama Saa Mbovu, Bugaja Rashid, Adam Maneno, Sawebu Juma na wengine saba bado hawajatambuliwa.
Aidha, majeruhi kumi na wawili wamepelekwa katika Hospitali ya Magunga, Wilaya ya Korogwe kwa ajili ya matibabu.