
Jeshi la Polisi limetahadharisha kuwa kuna kikundi cha watu ambao wanaandaa picha mjongeo na taarifa mbalimbali za matukio yaliyotokea siku za nyuma ambayo yalishashughulikiwa, na mengine ya kutunga ili wayasambaze kwenye mitandao ya kijamii yaonekane yametokea kipindi hiki au muda mfupi uliopita.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi imetahadharisha kuwa wapo pia walioandaliwa kama ambavyo baadhi wameshajitokeza kuzungumza na kutoa taarifa zenye tungo tata, zenye kutaka kuleta taharuki pamoja na kukusanya matukio ambayo yalitokea nchi zingine na kuyatengeneza kwa kuyawekea sauti zenye lafudhi ya Kiswahili ili yaonekane yametokea nchini.
“Pia wamepanga kuchukua picha za baadhi ya viongozi na kuyawekea maneno na sauti zenye matamko ya upotoshaji ili ionekane wao ndiyo wanazungumza au wanayatamka wakati si kweli,” imeeleza taarifa ya Polisi.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa raia kwa wananchi endapo wataona au kutumiwa picha mjongeo na taarifa kama hizo au vipeperushi na mengine yanayofanana na hayo wayapuuze kwani yameandaliwa kwa nia ovu ya kihalifu kwa lengo la kutaka kuleta taharuki kwa wananchi.







